KAIMU Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Ayoub Mohammed Mahamoud,
amesema lengo la serikali ni kuhakikisha sekta ya utalii inaimarika na
kuleta tija kwa nchi na wananchi wake.
Ayoub ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi, alieleza hayo
kwenye mkutano uliowakutanisha uongozi wa mkoa huo na wawekezaji wa
sekta ya utalii katika mkoa huo.
Ayoub aliwataka wawekezaji hao kuendelea kushirikiana na serikali
ambayo ina nia ya dhati ya kuzipatia ufumbuzi changamoto hizo sambamba
na kushirikiana na wananchi kwenye maeneo ya uwekezaji.
Alisema serikali itaendelea kutimiza wajibu wake wa kuweka mazingira
mazuri katika sekta ya utalii, lakini pia na wawekezaji wana haki ya
kutekeleza majukumu yao katika kuchangia kukuza sekta hiyo.
Katika hatua nyengine mkuu huyo aliagiza kutiwa ndani kwa kosa la
utovu wa nidhamu meneja wa shirika la Umeme (ZECO) Kanda ya kaskazini
Khamis Mbarouk Kitwana kwa kukaidi wito wa kutakiwa kushiriki katika
mkutano huo.
Mkuu huyo alimuita meneja huyo kwa ajili kutoa maelezo juu ya tatizo
la kukatika mara kwa mara kwa umeme katika maeneo ya hoteli za kitalii
katika eneo hilo.
Kwa upande wao wawekezaji hao wa hoteli za kitalii walisema
kutoimarishwa kwa miundombinu ya barabara, umeme, maji safi na salama
kwenye maeneo ya hoteli ni mongoni mwa mambo yanayoongeza gharama za
uendeshaji kwenye miradi yao.
Wakizungumza katika kikao cha pamoja na uongozi wa mkoa wa Kaskazini
Unguja katika ukumbi wa ofisi ya mkoa huo, huko Mkokotoni wamesema kuwa
matatizo hayo kwa kiasi kikubwa yamekuwa yakirudisha nyuma maendeleo ya
sekta hiyo.
Katika kikao hicho, wawekezaji hao waliiomba serikali kuhakikisha
inazifanyia kazi changamoto hizo za miundombinu ya kijamii ili mizgo wa
gharama za uendeshaji uweze kupungua.
Sorce Zanzibar leo